Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina na leo tunakwenda nchini Kenya ambako Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo imetoa tahadhari ya kwamba taifa hilo la Afrika Mashariki litakabiliwa El Nino kuanzia mwezi ujao wa Oktoba hadi Desemba mwaka huu wa 2026.

El Nino huweze kusababisha mvua kubwa na kwingineko ukame mkali. Kufuatia onyo hilo, tayari shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, (WFP) kwa kushirikiana na serikali wameanza kuchukua hatua za mapema ili kuepusha madhara makubwa. Sasa nini kinafanyika? Assumpta Massoi wa Idhaa hii, kupitia mahojiano yaliyofanywa na Mercy Korir, mwanafunzi wa vitendo kwenye kituo cha huduma za Habari cha Umoja wa Mataifa nchini Kenya, UNIS, ameandaa mada hii kwa kina. Pia tunakuletea muhtasari wa habari.

• Dunia inaingia katika kipindi ambacho upatikanaji usiotabirika wa maji unazidi kuwa kawaida, imeonya leo ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO. Ripoti hiyo inasema mwaka 2025 ulikuwa miongoni mwa miaka yenye mtiririko mdogo zaidi wa mito katika miongo mitatu na nusu. Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, amesema hali hiyo ni ishara inayoendelea kwa muongo mmoja. Akisistiza hilo Wayne Jenkinson, Mkurugenzi, Kitengo cha Hidrologia WMO anasema, “Mara nyingi maji hayapatikani mahali tunapoyahitaji, wala wakati tunapoyahitaji.” • Zaidi ya watoto 57,000 wameyakimbia makazi yao nchini Yemen katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kutokana na mapigano mapya, huku wengine wakiuawa, kujeruhiwa au kutoweka. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linaonya kuwa vurugu hizo zinazidisha janga la kibinadamu katika nchi ambako zaidi ya watoto milioni 12 wanategemea misaada baada ya zaidi ya muongo mmoja wa mzozo. Msemaji wa UNICE Joe English amesema watoto wengi nchini Yemen hawajui maisha mengine isipokuwa mzozo na kuhama kutoka kwenye makazi yao. Na kwamba “Hawa ni watoto ambao tayari wamepitia miaka ya njaa, kufurushwa makwao na migogoro, na sasa wanalazimishwa kuondoka tena katika makazi yao”. • Na Wanawake duniani kote bado wanapata kwa wastani asilimia 20 chini ya wanaume, licha ya juhudi za muda mrefu za kukuza usawa kazini. Katika Siku ya Kimataifa ya Usawa wa Mishahara, Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Kazi Duniani (ILO) na la masuala ya Wanawake UN Women yanasema pengo hilo si jambo lisiloepukika, na yanataka hatua kuhakikisha wanawake wanalipwa sawa kwa kazi zenye thamani sawa. ILO inasema “Usawa wa mishahara ni suala la haki, kanuni, utu na usawa wa kijamii – kwa kila mfanyakazi, kila mahali” wakati UN Women ikisisitiza kuwa “Usawa wa mishahara si suala la haki pekee; unaimarisha familia, uchumi na jamii.” Mashirika hayo yanasema sasa kinachohitajika ni hatua za kubadili ahadi za usawa wa mishahara kuwa uhalisia. Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Podden och tillhörande omslagsbild på den här sidan tillhör United Nations. Innehållet i podden är skapat av United Nations och inte av, eller tillsammans med, Poddtoppen.